Yesu Kristo napenda kuwakaribisha wote kutembelea na kujifunza mambo mbali mbali kuhusu Parokia yetu. Mpango kazi wa uchungaji na maendeleo kwa Parokia Teule ya Mt. Monica - Langoni ni mpango thabiti ambao uongozi wa kanisa umeweka likishirikisha maswala ya uchungaji na maendeleo ya watu.

Naomba baraka za Mungu tunapoelekea utekelezaji wa mipango hii nikitumaini kuwa dhima yetu ikiongozwa na dira vitaleta matokeo chanya kwa vile mipango hii inalenga katika kuhudumia na kulikomboa taifa lote la Mungu. 

Maombi na tamanio langu la dhati kwa Mungu ni kwamba namwomba atiririshe baraka zake tele katika juhudi zetu za kulije
nga taifa la Mungu, kiroho na kimwili katika safari yetu ya kiimani.

Nawashukuru kila mmoja kwa ushiriki wake katika kufanikisha matayarisho ya mipango mbali mbali na ninawaalika nyote kuitafsiri mipango hii kwa matendo kwa kushirikishana na kuhamasishana, kila muumini apate kushiriki na kuzifanya kazi hizi na utume kuwa mali, na wajibu wake.

Tafadhali tutumie nafasi hii muhimu tulio nayo katika kuliunga mkono kanisa kwa kukutumia yale yote mungu aliyotujalia kutimiza mipango mbali mbali ndani ya Parokia yetu Teule ya Mt. Monica - Langoni. (............maana huduma hii takatifu mnayoifanya si kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu tu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. 2Kor 9 : 12)

"KRISTU TUMAINI LETU UTUONGOZE"

Padre Beatus Vumilia
Padre Kiongozi
Parokia Teule Mt. Monica Langoni
Jimbo Katoliki Moshi

*HISTORIA YA VALENTINE  DAY* 

 _Inawajia kwa hisani ya Fr Beatus Vumilia,St. Monica -Langoni Elected Parish -Moshi._ 

Mtakatifu Valentino alikuwa ni padre wa Roma (Italia) ambaye aliishi kwa kuishuhudia imani ya kikristo kati ya mwaka 197 na 273. Kanisa linamtambua kuwa ni shahidi wa imani kwa kuwa alitoa uhai wake kwa kuilinda, kuitetea na kuitangaza imani ya kikristo. Lakini pia Mtakatifu Valentino anajulikana duniani kote kuwa ni mtakatifu wa wapendanao. Kwa hiyo utakatifu wake katika historia ya Kanisa na umaarufu wake duniani kote ni mambo mawili yanayojikitika katika jambo moja la msingi kwa maisha ya mtu wa dini yeyote na mahali popote; jambo hilo ni imani.

Valentino aliongoka katika ujana wake na kubatizwa mnamo mwaka 197 na baadae akawa Padri kwa kuiishi imani ya kikristo mpaka mwaka 273  alipouawa kwa ajili ya kuitetea imani. Imani hiyo ya kikristo aliishi si tu kwa maneno bali pia kwa vitendo kwani wakati ule kuwa mkristo ilikuwa ni jambo gumu sana. Ugumu huo ulitokana na ukweli kwamba watawala wa Kirumi wa nyakati hizo walikuwa bado hawajaipokea imani ya kikristo. Valentino aliishi imani ya kikristo nyakati za mfalme Claudio ambaye mara kadhaa alimtesa na kumfunga gerezani na baadae aliuawa kwa amri ya mfalme Aureliano. Utakatifu wake Mtakatifu Valentino anatambulika na wengi duniani pote kwa sababu ya upendo wake kwa watu. Tabia yake ya kupenda watu ilijikita katika imani yake kwa Neno la Yesu, “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yoh. 15:12-13).

Mtakatifu Valentino alitumia muda wake mwingi kuwasaidia watu wa ndoa na vijana wachumba kwa kuwafundisha juu ya upendo. Aliwafundisha kuwa upendo ni fadhila kuu ya kikristo na kiutu, kwa hiyo alisisitiza kuwa upendo ni kielelezo cha imani na utu. Watu wa ndoa aliwafundisha kuwa upendo wao hujionesha katika mambo makuu mawili: uaminifu na umoja. Uaminifu wa viapo vya ndoa katika kupendana na kuheshimiana siku zote na kwa hali zote. Umoja katika kutambua kuwa ndoa ni kati ya mume mmoja na mke mmoja. Mtakatifu Valentino aliishi nyakati ambazo ndoa za mume mmoja na wake wengi zilikuwa ni kama jambo la kawaida. Wanawake walinyimwa upendo ndani ya ndoa zao na wakawa wanyonge mbele za waume zao. Yeye alikemea jambo hilo bila kujali mtu yeyote; watawala kwa mfano, walikuwa pia na tabia hiyo ya kukosa uaminifu kwa ndoa zao. Polepole watu wengi walianza kujirekebisha na upendo ukaanza kurudi ndani ya ndoa. Hata hivyo mfalme Claudio alimchukia Valentino na kumfunga gerezani.

Wachumba aliwafundisha kuwa upendo wa kweli wa wapendanao hujidhihirisha katika kufunga ndoa mbele ya Mwenyezi Mungu. Hivyo basi aliwakemea bila woga vijana wengi waliokuwa wanaishi maisha ya unyumba. Vijana wengi waliongoka na kufunga ndoa takatifu kanisani. Jambo hili pia lilimkera sana mfalme kuona kwamba watu wengi wanaingia katika dini ya kikristo. Pia aliwatetea vijana waliokuwa jeshini ambao walikatazwa kwa sheria ya mfalme wasifunge ndoa. Sheria hiyo iliwanyima wanajeshi maisha ya ndoa kwa imani kuwa askari hodari hawatakiwi kuishi maisha ya ndoa.

Mtakatifu Valentino alipigania haki ya hao askari na kuwataka watawala waibatirishe sheria hiyo potovu. Katika kuwasaidia watu wautambue utakatifu wa ndoa, Mtakatifu Valentino alifanikiwa kuwafungisha ndoa wachumba wawili (mmoja mkristo na mwingine alikuwa mpagani) ambao wazazi wao walikuwa wamewawekea vikwazo. Mchumba wa kike ambaye ni mkristo alikuwa mgonjwa na yule wa kiume ambaye ni mpagani alikuwa ni askari. Askari aliwaambie eti si vizuri aoe kwani maisha yake yamo daima hatarini na hasa wakati wa vita na hivyo atamwacha mkewe kuwa mjane.

Na yule binti pia aliambiwa asiolewe eti kwa kuwa yeye ni mdhaifu na hivyo anaugua mara nyingi itakuwa ni vigumu kwake kutimiza wajibu wake wa nyumbani. Mtakatifu Valentino aliingilia kati na kuwafundisha wazazi wa vijana hao kuwa upendo hauna mipaka wala ubaguzi. Na pia wale wachumba akawafundisha kuwa katika ndoa ni lazima kupendana katika taabu na raha, afya na magonjwa, na kuheshimiana daima. Mtakatifu Valentino alifaulu kumbatiza askari na kumfungisha ndoa kwa yule binti ambaye alikuwa taabani mgonjwa kitandani.
Ushahidi wake Mnamo mwaka 269 mfalme Aureliano alimkataza rasmi Valentino kuhubiri, kuwaongoa na kuwafungisha ndoa takatifu. Mtakatifu Valentino aliendelea kumshuhudia Kristo bila woga na akawa tayari kwa lolote ila tu upendo wa Kristo uhubiriwe. Mwaka 270 mfalme alimhukumu Valentino adhabu ya kufungwa gerezani kwa miaka mitatu.

Urithi wake

Mtakatifu Valentino ametuachia urithi mkubwa wa imani. Mtakatifu Valentino anatufundisha kuwa fadhila ya upendo ni kielelezo cha imani. Mtu yeyote mwenye imani humpenda Mungu na huwapenda wenzake. Kipimo cha imani na kipimo cha utu ni upendo. Dunia inahitaji sana upendo ili mambo mengine mazuri yawezekane.
Mtakatifu Valentino alitambua kuwa watu wa familia wanapopendana jamii yote itapendana na kuishi kwa amani. Anatufundisha kuwa upendo huanzia nyumbani, yaani kati ya wanafamilia.
Ndiyo maana aliwataka watu wa ndoa wapendane katika misingi ya imani na wafunge ndoa takatifu.

Leo hii watu wengi duniani pote wanaikumbuka tarehe ya *14. FEBRUARY* kuwa ni siku ya wapendanao. Je, wanatambua kwa nini Valentino alitoa uhai wake siku hiyo?

Tunatakiwa tupendane kwa upendo wenye msingi katika imani kama alivyofundisha mtakatifu Valentino. Siku ya Mtakatifu Valentino ni siku ya wapendanao katika misingi ya imani na utu.
Kwa bahati mbaya watu wengi katika maisha ya leo tunapendana katika misingi ya tamaa za kimwili na kimapato. Leo hii kuna watu wengi wa ndoa ambao wana nyumba ndogo lakini nao wanasema eti leo ni siku yao ya WAPENDANAO. Ni upendo gani huo wenye nyumba kubwa na ndogo?
Je, Valentino hakufa kwa kupinga jambo hilo? Vijana wengi leo wanaishi uchumba sugu bila kufunga ndoa. Lakini wao pia wanasema eti leo ni siku yao ya wapendanao. Ni upendo gani huo pasipo msingi wa imani. Je, valentino hakutoa uhai wake ili kuwafundisha na kuwapigania vijana wafunge ndoa takatifu? Ni ajabu kuwa siku ya Mtakatifu Valentino uovu mwingi dhidi ya upendo ndiyo hufanyika. Ni vema siku hii iwe kwa ajili ya kujikumbusha maana halisi ya upendo. Wakati ule Mtakatifu Valentino alikwazika sana kuona watu wanaishi pamoja bila kufunga ndoa, alikwazika kuona vijana watu wa ndoa wanakosa uaminifu katika ndoa zao. Na alisikitika kuona hata vijana wanakosa haki za kuuishi upendo wa ndoa. Lakini akija leo hii, mtakatifu Valentino atashindwa hata kushangaa kuona jinsi upendo ulivyogeuzwa kuwa ni starehe ya kimwili badala ya kuwa ni fadhila ya kimungu.

Na mbaya zaidi atakutana na watu wa jinsia moja (ushoga na usagaji) wanaodai eti wanapendana na wana haki ya kufunga ndoa. Katika siku hiyo Mtakatifu Valentino   anatukumbusha tena kuwa upendo ni fadhila ya Kimungu na sio starehe ya kimwili.

HAPPY  VALENTINE DAY

RATIBA NA UTARATIBU WA UTOAJI WA VIPAJI KWA MWAKA 2022