Yesu Kristo napenda kuwakaribisha wote kutembelea na kujifunza mambo mbali mbali kuhusu Parokia yetu. Mpango kazi wa uchungaji na maendeleo kwa Parokia Teule ya Mt. Monica - Langoni ni mpango thabiti ambao uongozi wa kanisa umeweka likishirikisha maswala ya uchungaji na maendeleo ya watu.

Naomba baraka za Mungu tunapoelekea utekelezaji wa mipango hii nikitumaini kuwa dhima yetu ikiongozwa na dira vitaleta matokeo chanya kwa vile mipango hii inalenga katika kuhudumia na kulikomboa taifa lote la Mungu. 

Maombi na tamanio langu la dhati kwa Mungu ni kwamba namwomba atiririshe baraka zake tele katika juhudi zetu za kulije
nga taifa la Mungu, kiroho na kimwili katika safari yetu ya kiimani.

Nawashukuru kila mmoja kwa ushiriki wake katika kufanikisha matayarisho ya mipango mbali mbali na ninawaalika nyote kuitafsiri mipango hii kwa matendo kwa kushirikishana na kuhamasishana, kila muumini apate kushiriki na kuzifanya kazi hizi na utume kuwa mali, na wajibu wake.

Tafadhali tutumie nafasi hii muhimu tulio nayo katika kuliunga mkono kanisa kwa kukutumia yale yote mungu aliyotujalia kutimiza mipango mbali mbali ndani ya Parokia yetu Teule ya Mt. Monica - Langoni. (............maana huduma hii takatifu mnayoifanya si kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu tu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. 2Kor 9 : 12)

"KRISTU TUMAINI LETU UTUONGOZE"

Padre Beatus Vumilia
Padre Kiongozi
Parokia Teule Mt. Monica Langoni
Jimbo Katoliki Moshi

 MAMBO 20 NILIYOJIFUNZA 2022.

 Inawajia kwa hisani ya Fr Beatus Vumilia 
St. Monica -Langoni Elected Parish -Moshi.

1.        Mungu ni Mungu tu, hata kama huamini kuwa Mungu yupo yeye atabaki kuwa Mungu.

2.      Kuna siku yale waliyokufundisha/kuonya/kuelekeza wazazi/walezi wako utayashuhudia kwa macho yako mwenyewe.

3.      Unahitaji kujifahamu vizuri wewe mwenyewe, uhodari wako, udhaifu wako na uwezo wako wa katika Nyanja mbalimbali. Itakusaidia sana.

4.     Ukiweza kuokoa muda umepiga hatua kubwa sana maishani; mimi huona ukiweza kuokoa muda ni sawa na kushinda nusu ya vita unazotakiwa kupambana hapa duniani.

5.      Kuna watu kwenye maisha watakufanyia wema ambao kamwe huwezi kuwalipa.

6.     Kila mtu ana pande nne, uzuri, ubaya, ujasiri na udhaifu;  Hivyo ni juu yako kuchagua upande gani utautazama.

7.      Jitahidi kwa uwezo wako wote kuwa na amani na kila mtu/kuishi vizuri na kila mtu.

8.      Mahusiano yanahitaji muda, pesa, akili,na nguvu zako; kama haupo tayari usiingie.

9.     Unaweza kuwa mtu muhimu sana kwa mtu lakini sio muda wote; hivyo usijisahau soma alama za nyakati.

10.  Mtu ambae ni mwema kwako lakini ni katili(anafanya mabaya) kwa wengine; hata wewe hakufai.

11.     Tafuta taarifa/maarifa sahihi, muda mwingine unaweza kuhangaika sana na tatizo ambalo suluhisho lake linafahamika.

12.   Matumizi ya pesa yafanywe na akili yako na  sio moyo wako.

13.   Kuna nyakati mbaya zitakupata ili kukuokoa na nyakati mbaya zaidi zilizopo mbele yako; hivyo usilaumu kila jambo lina sababu.

14.   Wema/uzuri wako unaweza kukuingiza matatizoni pia; hivyo ukifanya jambo usitegemee mrejesho chanya pekee hataka umefanya mema.

15.   Muda mwingine ukicheka unaweza kueleweka vibaya hata kama hukucheka kwa ubaya; hivyo tabasamu zaidi kuliko kucheka.

16.   Jitahidi kuwaelewa watu kwa matendo yao kuliko kuwafahamu kwa maneno yao.

17.    Jitahidi katika mipango yako usimtegemee mwanadamu yeyote.

18.   Mahangaiko yote ya duniani ukifuatilia mwisho wa siku ni kutafuta furaha; hivyo fanya kile unachokipenda.

19.   Unaweza kutazama maisha ya mtu na ukajifunza somo kubwa ambalo vitabu havijapata kuandika, wahamasishaji hawajawahi kuongea na waigizaji hawajawahi kuigiza; *penda kujifunza kwa mifano inayoonekana.

20.Jifunze angalau kitu kimoja kila siku, kifupi usichoke kujifunza. Na zaidi ya yote jifunze kupitia makosa yako ili uzidi kukua siku hadi siku.