About Us

HISTORIA FUPI YA PAROKIA TEULE YA MT. MONICA - LANGONI 


HISTORIA YA AWALI

Eneo

Parokia Teule ya Mt. Monica – Langoni ipo upande wa Mashariki mwa Mkoa wa Kilimanjaro, Manispaa ya Moshi, kata ya Mji mpya takribani kilometa 8 kutoka Moshi mjini kupitia barabara ya Majengo. Eneo la Parokia teule lina ukubwa wa takribani ekari 6. Eneo hili linajumuisha jengo la Kanisa la mpito, nyumba ya Mapadre, jiko la nje, jengo la utawala, eneo la kilimo cha ndizi, mboga mboga na bwawa la samaki.
Kwa upande wa Kusini, Parokia Teule imepakana na msitu wa Rau, Mashariki ni barabara ya Langoni na msitu, Magharibi ni barabara ya Mji mwema, Kaskazini ni barabara kuu ya Langoni. Parokia za jirani ni Parokia ya Kristu Mfalme, Parokia Teule ya Mnazi, na Kituo cha Sala cha Msaranga.
Ujenzi wa Kanisa
Historia ya Parokia Teule Langoni inakuja kwa kuzingatia jitihada kubwa zilizofanywa na waamini katika maeneo ya Langoni kwani walipata shida kutokana na umbali wa kwenda kusali Parokia ya Kristu Mfalme. Kanisa lilipewa eneo na familia ya Mzee Alois Kiko Mlay mwaka 1992 na kukabidhiwa kwa Pd Agapiti Amani Aliyekuwa paroko wa KRISTO MFALME. 
Parokia Teule ya Mt.Monica–Langoni ilianza kama Kigango cha Parokia ya Kristo Mfalme-Moshi, kikijulikana kama Kigango cha Langoni mpaka ilipofika tarehe 16/6/2019 kilipofanywa rasmi kuwa Parokia Teule na aliyekuwa Msimamizi wa Jimbo la Moshi Padre Deogratias Matiika.
Kigango cha Langoni kilianzishwa tarehe 6/2/2011 kwa Ibada ya Misa ya kwanza ambayo iliadhimishwa na Padre Chrispine Jumanne, aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Kristu Mfalme na ndiye mwanzilishi wa Kigango cha Langoni. Ibada hiyo ilifanyika chini ya kivuli cha mti katika eneo la kiwanja ambacho kilitolewa na Mzee Aloisi Kiko Mlay tangu mwaka 1992.
Upatikanaji wa Ibada ya Misa katika Kigango cha Langoni kabla haijawa Parokia Teule ulikuwa ukibadilikabadilika kuendana na uhitaji wa waamini ulivyoongezeka. Mwanzoni, Ibada ya Misa ilikuwa inatolewa mara moja kwa mwezi, baadaye zikaongezeka zikawa mara mbili kwa mwezi, na baadaye Ibada ikawa inapatikana kila Dominica kutokana na mwamko wa waamini wa Langoni.
Kufuatia mwamko mkubwa wa waamini kiimani kuanzia January 2016 Ibada za Misa ziliongezeka na kuwa tatu kwa Dominica na pia Ibada za Misa kila siku ya juma zilianza kuwepo asubuhi saa 12:30. 

KAMATI TENDAJI YA KWANZA YA KIGANGO NA MCHAKATO WA KUFANIKISHA UJENZI WA KANISA LA MUDA (2011 - 2012) 
Kigango Kilifanya uchaguzi wa kamati tendaji ambapo,
 1. Bw. Severini Swai Alichaguliwa kuwa M/Kiti.
 2. Bi. Mary Tengia (Makamu M/kiti).
 3. Bw. Patrick Shirima (Katibu).
 4. Bw. James Shayo (Katibu Msaidizi).
 5. + Bw. Rogasiani Shao (Mhazini) baadae nafasi yake kujazwa na Bi Theodora Momburi.
 6. Bw. Albin Moshi (Mratibu wa JNNK). 
Kutokana na uhitaji wa nyumba ya Ibada, kamati tendaji pamoja na wanajumuiya wa JNNK zote walifanya bidi ya kujichangisha na kuomba kibali cha kujenga kanisa la muda kwa aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme. Paroko alipitisha ombi hilo na ujenzi ukaanza mwaka 2012 na kukamilika kwa haraka. Na mnamo mwaka 2012 kanisa la muda lilianza kutumika rasmi kwa ajili ya Ibada za Misa. Kamati tendaji iliendeleza utume na uendeshaji wa majukumu yake hadi 2019 ambapo ulifanyika uchaguzi wa kamati mpya ya parokia teule. 

MAPADRE WAHUDUMU KATIKA KIGANGO CHA LANGONI MPAKA SASA AMBAPO NI PAROKIA TEULE (2011-2020)

Mapadre waliohudumu katika Parokia Teule Langoni tangu ilipokuwa Kigango, Padre Chrispine Jumanne ambaye ndiye muasisi wa Kigango akisaidiwa na Padre Fulgence Sangawe kuanzia mwaka 2011-2012, Padre Paul Vumilia (2012-2014), Padre Calistus Msuri (2014-2016), na Padre Beatus Vumilia amekuwa Padre Mlezi kuanzia mwaka 2016 hadi tarehe 16/6/2019 ambapo Kigango cha Mt. Monica kilipanda hadhi na kuwa Parokia Teule na yeye akateuliwa kuwa Padre Kiongozi akisaidiwa na Padre Wilhelm Malasi (Padre Kiongozi-Msaidizi).

Parokia Teule ya Mt. Monica – Langoni inaundwa sasa na Kanda sita zenye jumuiya 34, Kanda hizo ni 
 1. Kanda ya NAZARETH, 
 2. Kanda ya BETHLEHEMU (Zamani Miembeni), 
 3. Kanda ya GALILAYA (Zamani Mji mwema),
 4. Kanda ya MALAIKA WALINZI (Zamani Mji Mpya “A”), 
 5. Kanda ya WATAKATIFU WOTE (Zamani Mjimpya “B”)  
 6. Kanda ya BETHANIA (Zamani Langoni.)
DIRA YETU
Kanisa katoliki Langoni kama familia ya Mungu inayoongozwa na amali za injili inawajibika kujenga malezi mfungamano na endelevu ya kiimani, kichingaji na kiuchumi katika mwanga wa tunu zifuatazo

 1. UWAZI
 2. UZALENDO
 3. UADILIFU
 4. UWAJIBIKAJI

DHIMA YETU  
Kanisa Katoliki Langoni litaendelea kujenga familia ya Mungu iliyoshikamana na kuwajibika kwa kushuhudia na kueneza habari njema ya wokovu na kutoa huduma za kijamii kwa uwazi, uzalendo, uadilifu na uwajibikaji.